NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
KOCHA MKUU wa Coastal Union ya Tanga, Yusuph Chippo amesema anaamini mipango ya timu hiyo ya kuchukua ubingwa wa Ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu yatatimia na hivyo lazima watanzania lazima wataipenda.
Coastal Union ya Tanga ni timu ambayo imeanza vema msimu mpya wa Ligi kuu soka Tanzania bara ambapo kwa sasa ina pointi 11 ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi kuu.
Alisema kuwa mikakati yake ni kuhakikisha kila mechi timu hiyo inapata matokeo mazuri yatayoiwezesha kufanikisha ndoto zao kufanya mapinduzi kwenye michuano hiyo ambayo inashirikisha timu kumi na nne.
Aidha alibainisha kuwa kikubwa ambacho anajivunia ni kuwa na kikosi madhubuti ambacho kimempa dira ya mafanikio mbeleni yanayotokana na usajili mzuri ambao timu hiyo ilifanya kabla ya kuanza msimu huu.
“Kwa hakika Coastal Hii lazima mtaipenda sasa tunajiandaa
kuwakabili wanaramaramba tukiwa na lengo moja tu la kupata pointi tatu muhimu ili kuweza kuendeleza rekodi yetu ya ushindi kama ilivyokuwa kawaida yetu “Alisema Chippo.
Akizungumzia mechi hiyo,Chippo alisema kuwa wachezaji wa timu hiyo wanaendelea na mazoezi ya kuhakikisha wanapata pointi tatu muhimu kwa sababu hilo linawezekana kutokana na wachezaji mahiri wanaounda kikosi cha Wagosi hao wakaya.
Coastal Union itaingia kwenye mechi yao na Azam Fc mwishoni mwa wiki ikiwa na kumbukumbu ya kupata matokeo mazuri kwenye mechi yao ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani.