Tuesday, December 16, 2014

“Coastal Union kukipiga na Mwadui FC ya Shinyanga Alhamisi Mkwakwani”


MABINGWA wa soka Tanzania Bara mwaka 1988 Coastal Union “Wagosi wa Kaya”inatarajia kucheza mechi ya kirafiki na Mwadui ya Shinyanga ikiwa ni sehemu ya maandalizi kwa timu zote kujiandaa na michuano wanayokabiliana nayo.


Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Alhamisi ya wiki hii kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani lengo likiwa ni kukipa makali kikosi cha Coastal Union kujiwida na mechi yao ya Ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Tanzania Prison itakayochezwa kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.


Akizungumza na Coastal Union Official Site,Katibu wa Coastal Union,Kassim El Siagi alisema kuwa mechi hiyo ni miongoni mwa michezo mbalimbali ya kirafiki wanayocheza ili kuweza kukiimarisha kikosi hicho ambacho msimu huu kimepania kufanya makubwa kwenye michuano ya Ligi kuu soka Tanzania.


El Siagi alisema kuwa timu ya Mwadau ya Shinyanga inatazamiwa kuwasili mkoani hapa Jumanne wiki hii tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao unatazamiwa kuwa na upinzani mkali.


Hata hiyo aliwataka wadau wa soka mkoani hapa kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo ikiwemo kuangalia wachezaji ambao wamesajiliwa msimu huu kwa ajili ya michuano ya Ligi kuu soka Tanzania bara.


   “Tunawajua Mwadui FC sio timu mbaya hivyo naamini kutakuwa na burudani ya kukata na shoka nawasihi wakazi wa mkoa wa Tanga wajitokeza kwa wingi ili kushuhudia mchezo huo “Alisema El Siagi.


Hata hivyo alisema kuwa baada ya kumalizika mechi hiyo wataangalia uwezekano wa kucheza mechi nyengine ya kirafiki kabla ya kutua jijini Mbeya ambapo watakwenda kucheza mechi yao ya Ligi kuu.

No comments:

Post a Comment