Tuesday, October 21, 2014

COASTAL UNION YAANZA KUIPIGIA HESABU KAGERA SUGAR


TIMU ya Coastal Union ya Tanga imeanza maandalizi ya kuelekea mechi yao na Kagera Sugar itakayopigwa wikiendi hii kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba ikiwa ni muendelezo wa Ligi kuu soka Tanzania bara.
Kauli hiyo ilitolewa na Kocha Mkuu wa Coastal Union,Yusuph Chippo mara baada ya kumalizika mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea kwenye viwanja wa shule ya Sekondari Popatlaly mjini hapa.
Alisema kuwa kikosi chake kipo imara kuweza kuwavaa wakata miwa wa bukoba kutokana na kuimarisha sehemu mbalimbali kwenye timu hiyo hasa mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi yao na Mgambo Shooting ambapo Coastal ilishinda bao 2-0.
Kocha huyo alisema kuwa wembe uliotumika kuwanyoa timu hiyo ya Mgambo Shooting ndio ambao watautumia ili kuweza kupata pointi tatu muhimu wakiwa ugenini lengo likiwa kuweza kuwa kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi kuu .
“Tunamshukuru mungu kwa kupata pointi tatu muhimu kwenye mechi hii na hili linatokana na kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi yetu iliyopita lakini kubwa ni umoja na mshikamano uliopo “Alisema Chippo.

Hata hivyo aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanapambana vilivyo kila mchezo ili waweze kupata matokeo mazuri yatakayowawezesha kuirudishia heshima timu hiyo yenye maskani yake barabara 11 jijini Tanga.
Katika hatua nyengine,Timu hiyo inatarajiwa kutumia usafiri wa ndege kuelekea mkoani Kagera kucheza mechi yake ya Ligi kuu wikiendi hii dhidi ya Kagera Sugar mechi itakayochezwa uwanja wa Kaitaba.

No comments:

Post a Comment