Thursday, October 9, 2014

COASTAL UNION YAIFUNDISHA SOKA PANONI FC YA KILIMANJARO,YAICHAPA MABAO 2-1,MKWAKWANI.

                      


TIMU ya Coastal Union “Wagosi wa Kaya”jana waliendelea vema na maandalizi ya mechi zake zilizosalia katika michuano ya Ligi kuu soka Tanzania bara baada ya kuibamiza mabao 2-1 timu ya Panoni FC ya Kilimanjaro mchezo ambao ulichezwa uwanja wa CCM Mkwakwani.


Mchezo huo wa kirafiki ambao ulikuwa na burudani ya aina yake kutokana na timu zote kuonyesha kandanda nzuri na la kuvutia ambapo bao la kwanza la Coastal Union lilifungwa na Keneth Masumbuko dakika ya 23.


Bao hilo lilidumu mpaka timu zote zinakwenda mapumziko ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu.


Wakionekana kujipanga vilivyo baada ya kufanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji wake,Coastal Union waliweza kuutawala mchezo huo kwa kipindi hicho huku wakicheza pasi fupifupi na ndefu hali iliyopeleka kuandika bao la pili dakika ya 68 kupitia Omari Mahamudi “Hanzy”


Baada ya bao hilo kuingia langoni mwao, Panoni FC waliweza kubadilika na kucheza kwa umakini mkubwa hali iliyopelekea kupata bao la kufutia machozi kwenye dakika ya 82 kupitia Laurance Mbawa “Tevez”.


Akizungumza mara baada ya kumalizika mchezo huo,Kocha Mkuu wa Coastal Union,Yusuph Chippo aliwapongeza wachezaji wake kwa kupata ushindi lakini akiwasihi kuhakikisha wanakuwa makini kwenye mechi za ligi kuu ikiwemo kucheza kwa hari kubwa ili kuweza kupata pointi tatu muhimu.


Coastal Union inatarajiwa kucheza na Mgambo Shooting zote za jijini Tanga ikiwa ni Daby ya Tanga ambayo inatazamiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na historia ya timu hizo mbili.

No comments:

Post a Comment