Thursday, September 11, 2014

“SIMBA HAITUPI WASIWASI”

NA MWANDISHI WETU, TANGA.
TIMU ya Coastal Union ya Tanga leo imeendelea na mazoezi yake katika viwanja vya shule ya sekondari Popatlaly huku Kocha Mkuu wa timu hiyo,Yusuph Chippo akisisitiza kuwa mechi yao ya ufunguzi wa  Michuano ya Ligi kuu soka Tanzania bara baina yao na Simba haimpi wasiwasi wale kumnyima usingizi kutokana na uwezo mzuri wa kikosi chake.
Coastal Union iliyokuwa imeweka kambi visiwani Pemba takribani mwezi mmoja uliopita ilirejea mkoani hapa kwa kishindo na kuweza kuibamiza Polisi Morogoro mabao 2-0 mchezo wa kirafiki uliochezwa uwanja wa CCM Mkwakwani.
Ushindi huo na kiwango walichonacho wachezaji wa timu hiyo ndio kitu pekee ambacho kinampa jeuri Kocha huyo kutoa kauli hiyo kutokana na kikosi hicho kukamilika kila idara hasa ukizingatia na usajili walioufanya msimu huu.
Akizungumza mara baada ya kumalizika mazoezi hayo jana, Kocha Chippo alisema baada ya kufanya vizuri kwenye mechi zao za maandalizi ya kuelekea ligi hiyo sasa wana matumaini makubwa ya kuweza kuchukua pointi tatu kila mechi wakianzia na Simba itakayochezwa Septemba 20.
   “Unajua ligi kuu msimu huu itakuwa na ushindani sana kutokana na maandalizi yaliyofanywa na timu zote zinazoshiriki likini nasi pia tumejithatiti vilivyo kuweza kukabiliana na ushindani huo kwa kupata pointi tatu kila mechi “Alisema Chippo.
Hata hivyo aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanazingatia nidhamu ya hali ya juu wanapokuwa kwenye mechi zao za ligi kuu ili kuweza kupata ushindi mnono.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment